Serikali imesema imeanza hatua za kujenga ukuta katika eneo la Nungwi Zanzibar kwa ajili ya kusaidia kuzuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema hayo wakati akijibu swali la nyongeza Bungeni jijini Dodoma hii leo Februari 1, 2024, la Mbunge wa Nungwi, Simai Hassan Sadiki aliyetaka kujua kama eneo hilo limekidhi vigezo vya kujengewa ukuta, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema, “Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza miradi ya ujenzi wa kuta katika fukwe mbalimbali za bahari Tanzania Bara na Zanzibar. Eneo ambalo linapaswa kujengwa ukuta limekidhi vigezo na lina kila sababu ya kufanyiwa hivyo, tumeanza kufanya utafiti na tumeombea bajeti.“

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis.

Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Naibu Waziri Khamis alisema kuwa Serikali itaendelea kubaini maeneo yenye changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na kuyaweka katika kipaumbele ili kuyatafutia rasilimali fedha kwa ajili ya kuitatua.

Amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanazidi kusababisha athari katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya ukanda wa pwani nchini na kwamba Serikali inafanya tathmini ya kiwango cha uharibifu na athari zitakazojitokeza hii ni moja ya sababu ya mojawapo ya vigezo vinavyotumika kuweka vipaumbele maeneo yaliyoathirika katika mipango ya utekelezaji.

Hata hivyo, amewataka Wananchi kuacha kufanya shughuli zinazoharibu mazingira ya visiwa zikiwemo uvuvi usio endelevu na kilimo cha mwani kinachoharibu mazingira.

Geita Gold kuiwahi Simba SC Mwanza
Mradi upelekaji Umeme wa Gridi Rukwa umeanza - Kapinga