Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewaasa wananchi kuendelea kutoa maeneo yao, ili kuruhusu miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme ifike maeneo yote.

Kapinga ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Masimba, Kata ya Tongwe Wilayani Muheza Mkoani Tanga, katika ziara ya kukagua maendeleo ya Utekelezaji wa Miradi ya Usambazaji Umeme Vijijini.

Amesema, “Wananchi tushirikiane na Serikali, kuhakikisha umeme unafika kwenye maeneo yote nchini, niwashukuru wale wote wanaotoa maeneo yao kuruhusu miundombinu ya kusafirish na kusambaza umeme inapita ukizingatia miradi hiyo haina fidia.”

Aidha, Kapinga amewasisitiza Wananchi kuendelea kutandaza nyaya katika nyumba zao na kuwahakikishia kuwa umeme utamfikia kila Mtanzania kwa kuwa Serikali imetenga fedha nyingi za kutekeleza suala hilo.

Amewakumbusha pia Wakala wa Nishati Vijijini – REA, na Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO, kuzungumza na Wakandarasi wanaofanya kazi ya kusuka nyaya katika maeneo ya vijijini, kuwapatia wananchi gharama nafuu, ili waweze kumudu gharama.

Kuhusu mgao wa Umeme, Kapika amesema tatizo hilo ni la muda mfupi na litakwisha hivi karibuni kwa kuwa TANESCO inaendelea kuboresha miundombinu kwa lengo la kuimarisha upatikani wa huduma hiyo.

Mkoa wa Tanga una jumla ya Vijiji 779 ambapo Vijiji 701 tayari vina Umeme, Vijiji vilivyosalia vitaunganishwa na huduma hiyo kabla ya Mwezi Juni 2024, kupitia Miradi 4 inayoendelea mkoani humo.

Jaribio la mapinduzi lamfikisha Rais mstaafu Polisi
Familia zaelimishwa kinga magonjwa ya mlipuko Hanang'