Uongozi wa Geita Gold FC umesema upo tayari kwa mchezo wa Kiporo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba, utakaopigwa Februari 12 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Simba SC itaendelea na Ligi Kuu keshokutwa Jumamosi (Februari 03) kwa kucheza dhidi ya Mashujaa FC mjini Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika, kisha itarejea jijini Dar es salaam kupambana na Azam FC Februari 09 na kisha itaelekea Mwanza kukipiga na Geita Gold FC Februari 12.
Msemaji wa Geita Gold FC, Samwel Dida amesema baada ya kuona ratiba ilivotolewa na Bodi ya Ligi Kuu, akili yao yote kwa sasa imeelekea katika mchezo dhidi ya Simba.
Dida amesema wanaupa umuhimu mkubwa mchezo wao huo, hivyo wanafanya maandalizi ya kurejea mapema Mwanza kujipanga.
Amesema wanahitaji kuweka nguvu katika mchezo huo na mingine ijayo kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Ratiba inaonesha tuna mchezo Februari 12, mwaka huu, bado tupo kambini Morogoro tunafanya maandalizi ya mwisho kabla hatujarudi Mwanza kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba SC ambao huenda ukawa mgumu kulingana na ubora wa wapinzani, tunahitaji kuwa imara zaidi,” amesema.
Amesema malengo waliyoweka kuelekea lala salama ya Ligi Kuu ni kufanya vizuri katika michezo yote iliyobaki na hilo lazima litimie kwa sababu wana kikosi kizuri na wameshafanyia marekebisho chini ya Kocha mpya, Denis Kitambi.
Msimamo wa ligi unaonesha Geita iko katika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 16 baada ya kucheza michezo 13, kushinda minne, sare nne na kupoteza mitano.