Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili Serikali Nchini imetumia shilingi 1.29 trilioni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, ambapo kati ya fedha hizo shilingi 454.3 bilioni zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za elimu ya awali na msingi, ambapo jumla ya shule mpya zilizojengwa ni 342, vyumba vya madarasa 9,189, nyumba za walimu 346, mabweni 28 na ukarabati wa shule kongwe 45.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Februari Mosi, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Amesema, utekelezaji wa mtaala mpya umeanza katika ngazi ya Elimu ya Awali, Elimu ya Msingi – Darasa la I na III, Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza katika baadhi ya fani za amali katika shule 96 za Serikali na Binafsi ambazo zina miundombinu wezeshi kama karakana na Walimu wa fani hizo.
Majaliwa ameongeza kuwa shilingi 837.8 bilioni zimetolewa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zimetumika katika ujenzi wa shule za Sekondari mpya 486, vyumba vya madarasa 21,990, nyumba za walimu 280, mabweni 221, ukarabati wa shule kongwe 21, maabara 151 na mabwalo 23.