Kocha Msaidizi wa Simba SC Seleman Matola amesema kurejea kwa Kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chama ni faida kubwa kwa kikosi cha klabu hiyo kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi (Februari 03) dhidi ya Mashujaa FC.
Simba SC itakua ugenini katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ikicheza mchezo huo wa Kiporo, baada ya kurejea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara iliyokuwa imesimama kupisha Michuano ya Kombe la Mapinduzi na Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’.
Matola amesema Chama huenda akawa sehemu ya kikosi cha Simba SC katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa soka Mkoni Kigoma na maeneo ya karibu.
“Kurejea kwa Chama baada ya kumaliza matatizo yake ni faida kwa timu, ni mchezaji mzuri, ninaamini kama atacheza ataweza kuisaidia timu, kutokana na upinzani ambao tunautarajia kutoka kwa wapinzani wetu.”
“Kikosi kipo tayari kwa mchezo huo na kila mchezaji aliyekuja hapa Kigoma yupo FIT kwa ajili ya kupambana na tunatarajia kesho tukiamka salama, maamuzi yatabaki kwa kocha nani ataanza katika kikosi cha kwanza.” amesema Matola
Simba SC imetangaza kumsamehe Chama mapema leo Ijumaa (Februari 02) na tayari Kiungo huyo ameshaanza safari ya kuelekea Kigoma sambamba na Meneja wa Habari na Mawasilino Ahmed Ally.