Serikali Nchini, inakamilisha kazi ya uandaaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo Mwaka 2033 huku ikitatua vikwazo vya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wake, vifaa na majiko sanifu ya kupikia..

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga hii leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Jacqueline Ngonyani Msongozi (Viti Maalum), aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuweka ruzuku kwenye Nishati ya Gesi, ili Wananchi waweze kumudu na kutumia nishati hiyo.

Akijibu swali hilo, Kapinga amesema, “Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni Ajenda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na hilo lilitiliwa mkazo katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliofanyika Dubai. Hivyo Wizara ya Nishati inalibeba suala la nishati safi ya kupikia kwa uzito mkubwa.”

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Kuhusu ruzuku katika mauzo ya mitungi ya gesi, Naibu Waziri amesema tayari kuna programu na miradi mbalimbali inayoendelea akitolea mfano programu ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU) ambapo Mawakala wanawezeshwa kifedha ili kupunguza bei ya mitungi ya gesi kwa watu wanaonunua mitungi hiyo kwa mara ya kwanza na kwamba Serikali itaendelea kubuni miradi na kutafuta fedha ili wananchi wapate gesi kwa gharama nafuu.

Aidha, Kapinga ameongeza kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeanza mradi wa kusambaza nishati safi ya kupikia kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo magereza, kambi za jeshi, shule za msingi na Sekondari na kwamba zoezi hili ni endelevu na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuzifikia taasisi nyingi zaidi.

Matola achekelea msamaha wa Chama
Matola: Fanyeni subra mtafurahi