Mabingwa mara 22 wa Ligi Kuu ya Rwanda, APR wako katika mazungumzo ya kina ili kupata huduma ya kiungo Abraham Siankombo kutoka Zesco United ya Zambia kabla ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa mwaka 2024/2025.

Taarifa zinasema kuwa mazungumzo yanaendelea kati ya kikosi cha Jeshi na Siankombo ambaye pia anasakwa na Klabu ya Ajax Cape Town ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, mchezaji huyo wa kimataifa wa Zambia anafuatiliwa na mabingwa hao wa Rwanda pamoja na mshambuliaji wa Read Arrows, Ricky Banda.

Aidha, klabu hiyo inatarajia kuongeza nafasi ya kufanya vyema zaidi katika mashindano ya soka ya klabu Barani Afrika msimu ujao.

“Tunatazamia kuwasajili wawili hao na tunawajumuisha kwenye kikosi chetu kitakachoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika. Tuna majina mengine ambayo tunaamini yataisaidia klabu,” kilisema chanzo hicho.

Siankombo mwenye umri wa miaka 26, anachezea timu ya taifa ya Zambia huku Banda akiichezea timu ya Zambia ya chini ya umri wa miaka 23.

APR FC wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda msimu wa mwaka 2023-2024 na wamejikatia tiketi moja kwa moja kuiwakilisha Rwanda kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao.

Mabingwa hao sasa wanaongeza damu mpya katika kikosi chao katika juhudi mpya za kuboresha kikosi chao katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mwenyekiti wa APR FC, Richard Karasira alibainisha kuwa klabu hiyo ipo sokoni na kuna mazungumzo yanaendelea na wachezaji kadhaa.

Aliwahakikishia mashabiki wake kwamba watajenga timu imara ambayo itakuwa katika kiwango cha juu.

Hayo yametokea baada ya kocha mkuu wa klabu hiyo, Thierry Froger kuweka wazi kuwa kikosi cha sasa hakitoshi kutoa upinzani katika soka la Afrika.

APR ilifanya vizuri zaidi katika mashindano makubwa ya Afrika msimu wa mwaka 2004 wakati walipofikia raundi ya tatu timu hiyo ikiwa chini ya Jean Marie Ntagwabira (sasa marehemu).

Tangu wakati huo, klabu hiyo inayomilikiwa na jeshi, ilichukuliwa kuwa klabu yenye mafanikio makubwa na imekuwa ikishiriki mashindano makubwa ya klabu Barani Afrika.

Kipara anaomba muda zaidi Man Utd
Serikali kuunda timu tatu AFCON 2027