Mke wa Hayati Kapteni John Komba, Salome Komba amesema hahusishi kifo cha mumewe maadui zake wala sababu za kisiasa bali ni mapenzi na MUNGU kwani akiamua kukuchukua basi anafanya hivyo muda na mahali popote na kwamba alikuwa na hekima katika uamuzi wa mambo na alitenda haki hivyo wakati wake ulifika.

Salome ameyaema hayo hivi karibuni wakati akifanya Mahaojiano maalum na Dar24 Media na kuongeza kuwa hata baada ya msiba bado marafiki wa karibu wa Komba waliendelea kuwasiliana na kushirikiana na familia yake, kitu ambacho kinaonesha aliishi vizuri na watu bila migogoro ama migongano ya kimaslahi.

Amesema, “hapana kwakweli hata kama nisingeyasikia MUNGU ana siku yake ya kukuchukua, kwahiyo ikifika siku yako ya kukuchukua akisema leo nakuchukua hata hivi tulipokaa hapa akisema nakuchukua anakuchukua kwahiyo tusipingane na kazi ya MUNGU naona kile kipindi kilifika kwamba tarehe 28 mwezi wa 2, 2015 kwamba atatwaliwa.”

Jibu la Mke wa Komba lilikuja kufuatia swali wa Mwandishi wa Dar24 Media, Stanslaus Lambat kutaka kujua kama alisikia minong’ono ya kifo cha mumewe kwamba kilitokana na yeye kuwa na maadui wa kisiasa au watu wasiompenda ambao walifanya namna ili Komba atangulie mbele za haki.

Kuhusu mgogoro katika mgawanyo wa mali, Salome amesema, “Kapteni alikuwa anaona mbele sana, ilikuwa mwaka 2009 aliniita akachukua karatasi maalum za Bunge akaandika wosia kwamba nikifa leo au kesho mali zangu zote nimechuma na mama Salome hivyo namuachia yeye, na aliorodhesha na watoto watoto watano tuliozaa na wengine sita ambao sikuzaa naye lakini nimemkabidhi naomba aendelee kuwalea, kwakweli sikupata shida.”

Kapteni John Komba alizaliwa Machi 18, 1954 na baadaye alijiunga na jeshi mara baada ya masomo yake na kisha kujiingiza katika sanaa akiwa Mwimbaji mahiri na maarufu, kisha kujiingiza katika siasa, akawa Mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi – CCM. Alifariki Februari 28, 2015.

MAKALA: Utata ndani ya Kiongozi bora, bora Kiongozi
Malimwengu: Ukimuona Mkubwa lala chini, ni heshima.