Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Theopista Mallya amewataka waamini wa Kanisa la Moraviani Usharika wa Sogea Mjini Tunduma, kutojiingiza kwenye madeni makubwa ambayo hupelekea madhara ya msongo wa mawazo baada ya kushindwa kulipa madeni hayo.
Akizungumza na waumini wa Kanisa Moravian kwa Mchungaji Emmanuel Silungwe wakati wa ibada ya jumapili, Kamanda Mallya amesema madeni makubwa ni changamoto kwani husababisha msongo wa mawazo.
“Kitendo cha baadhi ya waamini kukopa mikopo mikubwa ambayo wanashindwa kumudu malipo yake kinapelekea kuwa na msongo wa mawazo na baadhi yao kujiua” alisema Kamanda Mallya.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mallya amewaomba waamini wa kanisa hilo kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, pamoja na kuacha vitendo vingine visivyompendeza Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wao baadhi ya waamini wa Kanisa hilo wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa ushiriki wao katika ibada hiyo na kutoa elimu ambayo ni sehemu ya mafundisho mema ikiwa ni pamoja na kufanikisha zoezi la harambee la kupaua jengo la ofisi ya Kanisa hilo ambalo ujenzi wake bado unaendelea.
Utoaji huo wa elimu katika nyumba za ibada ni mkakati wa Jeshi la Polisi kuhakikisha Viongozi wa Dini wanakuwa sehemu ya kuukataa uhalifu nchini na kutumia nafasi zao katika mahubiri kutoa elimu na kukemea vitendo viovu katika jamii.