Ili Tanzania iweze kufikia malengo ya Maendeleo iliyojiwekea, lazima iwe na Sera Bora ya Mambo ya Nje inayozingatia maoni na matakwa ya makundi yote ya wadau nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Ikulu Zanzibar, Ali Suleiman Ameir ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la wadau la kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 lililofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip mjini Zanzibar tarehe 05 Februari 2024.
Kongamano hilo ambalo ni la tatu kufanyika ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kushirikisha wananchi kutoa maoni yatakayozingatiwa katika zoezi la kurekebisha Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001.
Dhamana ya usimamia Sera hiyo ni ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ambaye ametaja sababu za Wizara yake kuratibu makongamano hayo ambapo alisema linalofuata litafanyika Pemba tarehe 10 Februari 2024.
Alisema, kufanyika kwa makongamano hayo ni utekelezaji wa misingi ya utawala bora ambayo inasisitiza umuhimu wa kushirikisha wadau katika utungaji wa Sera za nchi, ikiwemo Sera ya Mambo ya Nje.
Alieleza pia kuwa Sera ni Tamko linalotoa mwongozo namna nchi itakavyoshughulikia ushirikiano na uhusiano wake na dunia. Hivyo, utungaji wa Tamko muhimu kama hilo lazima lishirikishe wadau wote.
Makamba aliwambia washiriki wa Kongamano hilo kuwa Tanzania ina ushawishi mkubwa duniani tofauti na nguvu zake za kiuchumi na kijeshi kutokana na kuwa na Sera bora ya Mambo ya Nje. Hivyo, ili iendelee kuwa na ushawishi huo duniani lazima itungwe Sera imara itakayozingatia maoni ya wadau wote.
“Sera ya Mambo ya Nje ina uhusiano wa moja kwa moja na malengo ya Maendeleo ya nchi. Hivyo, mchakato wa utungaji wa Sera ya Mambo ya Nje lazima ushirikishe wadau kwa kuwa maendeleo ni jambo linalomgusa kila mmoja,” alisema.
Aidha, alihitimisha hotuba yake kwa kutaja baadhi ya mambo yaliyosababisha Serikali kufanya marekebisho ya Sera hiyo. Mambo hayo ni pamoja na mabadiliko yanayotokea duniani kama mabadiliko ya tabianchi, uvumbuzi wa teknolojia mpya, kuibuka kwa wadau wapya wa maendeleo wenye nguvu na ushawishi na Watanzania wengi hawakuwepo wakati wa utungaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001.
Kongamano hilo, limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Mustafa Kitwana, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Ikulu Zanzibar, Salehe Juma Mussa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Balozi Stephen Mbundi, Naibu Katiibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa, Mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi, Mabolozi Wastaafu akiwemo Balozi Amina Salum Ali, viongozi wa Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia, Wakuu wa taasisi za Serikali na Sekta Binafsi, Wakuu wa Vyombo vya habari, wanazuoni na wananchi kwa ujumla.