Kiungo Mpya wa Simba SC, Edwin Balua amesema anaiona nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza licha ya ushindani mkubwa uliopo katika timu hiyo.
Balua amesema muda mfupi tangu ajiunge na miamba hiyo amebaini kiwango alichonacho anaweza kulishawishi Benchi la Ufundi na kumpa nafasi.
“Nafasi yangu ya kucheza kikosi cha kwanza Simba SC, naiona nipo tayari kwa mapamano na kufanya kila nitakachoelekezwa na makocha, sihofii ukubwa wa majina niliyoyakuta hapa sababu mpira siyo majina,” amesema Balua.
Kiungo huyo aliyejiunga na Simba SC kwenye dirisha dogo akitokea Tanzania Prisons, amesema kitu cha msingi kwake ni kupambana na kumheshimu kila mtu hiyo ndio silaha kubwa kwake.
Amesema anajua kucheza Simba SC, kuna Presha kubwa kutokana na mashabiki kuhitaji ushindi na kiwango bora hivyo vyote amejipanga kuvukabili na anaamini atawafurahisha mashabiki zake,
Amesema anataka kuitumia Simba SC, kupandisha jina na kiwango chake na kuwa mchezaji mkubwa siku za baadae na hilo linawezekana kutokana na malengo yake.
Licha ya matumaini hayo lakini Balua anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa nyota wa kimataifa, Willy Esomba Onana pamoja na Saido Nibazonkiza ambao ndio chaguo la kwanza la kocha wa Abdelhak Benchikha.