Wabunge watatu wa upinzani wamekamatwa nchini Senegal, huku kukiwa na mzozo mkali wa kisiasa baada ya Bunge kupiga kura ya kuahirisha uchaguzi wa urais hadi Desemba 15, 2024.
Hatua ya kupitishwa muswada huo uliotekelezwa na Wabunge 105 kati ya 165, ilitajwa na upinzani kuwa ni mapinduzi ya kikatiba na kwamba utawala unaeondelea kuwa madarakani hauna tofauti na udikteta.
Miongoni mwa wabunge hao, yumo Guy Marius Sagna ambaye alijaribu kuzuia zoezi la kuupigia kura mswada huo, huku Msemaji wa Chama cha Upinzani kilichofungiwa cha Pastef, El Malick Ndiaye akisema ni wazi sasa Senegal imeingia katika utawala wa kidikteta.
Hatua ya kuahirisha uchaguzi, imesababisha maandamano makubwa katika miji kadhaa pamoja na kuzua wasiwasi wa kimataifa kuhusu mustakabali wa nchi hiyo, ambayo inachukuliwa kama kinara wa demokrasia eneo la Afrika Magharibi.