Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah Baresi’ amesema watatumia mbinu za Ihefu FC kuwafunga Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans.

Mashujaa inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kesho Alhamis (Februari 08) itakuwa mgeni wa Young Africans katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam Kocha huyo amesema wanalazimika kutumia mbinu zitakazowapa ushindi ili kujiondoa kwenye nafasi mbaya waliyopo sasa.

“Ukweli tunakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya vinara na mabingwa watetezi lakini tumepanga kutumia mbinu za Ihefu ambayo ndiyo timu pekee iliyoifunga Young Africans msimu huu,” amesema Baresi.

Kocha huyo kutoka visiwani Zanzibar ambaye timu yake ilipoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba SC, amesema anaridhishwa na upambanaji wa kikosi chake ambacho kina wachezaji waliosajiliwa kwenye dírisha dogo na anaamini nafasi ya kufanya vizuri kwao ni kubwa.

Amesema kinachowasumbua kwa sasa ni kupata ushindi wa kwanza utakaowajengea kujiamini na wamepanga kulifanya hilo.

Baadhi ya nyota waliosajiliwa na Mashujaa kwenye dirisha dogo ni pamoja na Reliant Lusajo, Balama Mapinduzi, Eric Johora, Zuber Dabi, Ibrahim Ame na Abrahaman Mussa.

Tulinde vyanzo vya Maji - Twaha Kiduku
Wabunge watatu wa upinzani wakamatwa