Kocha Mkuu wa Arsenal Mikel Arteta hatakumbana na adhabu yoyote kutokana na ushangiliaji wake wa ‘kikuda’ baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo wao wa Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool, Jumapili iliyopita, imeelezwa.
Lakini, Arsenal itakumbana na faini ya Pauni 25,000 baada ya wachezaji wake sita kuonyeshwa kadi za njano katika mechi hiyo ya ushindi wa mabao 3-1 uwanjani Emirates.
Arteta aliwachukiza baadhi ya mashabiki wa Liverpool kutokana na namna alivyoshangilia bao la tatu lililofungwa na Leandro Trossard kwenye dakika za majeruhi.
Kocha huyo Mhispaniaola alirukaruka kabla ya kukimbia kasi kutoka kwenye eneo lake na kuonyesha furaha utadhani ameshinda taji kubwa.
Lakini, kanuni za FA, zinaliacha suala la mambo ya kwenda benchi la ufundi kwa waamuzi wa uwanjani.
Na hakuna mwamuzi yeyote si Anthony Taylor wala aliosaidiana nao kwenye mechi hiyo, alionyeshwa kutofurahishwa na ushangiliaji wa Arteta, jambo ambalo FA haiwezi kuingilia kati.
Lakini, kadi za njano walizoonyeshwa mastaa Ben White, Gabriel, Jakob Kiwior na kwenye dakika za majeruhi William Saliba, Declan Rice na Kai Havertz, itawaweka kwenye matatizo makubwa Arsenal.
Liverpool ilishuhudia beki wake Ibrahima Konate akitolewa nje baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano, muda mfupi kabla ya Trossard kufunga bao la tatu kumaliza mechi.
Waliokerwa na ushangiliaji wa  Arteta ni wengi akiwamo gwiji wa Liverpool, Jamie Carragher alisema: “Aende zake vyumbani.
Ameshinda mechi. Ni pointi tatu tu hizo. Sawa, wamerudi kwenye mbio za ubingwa, lakini angeenda tu vyumbani.”
Mchambuzi mwenzake, beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville alisema: “Kushangilia ule ni utoto.”