Wakati Chama cha Soka nchini Ghana ‘GFA’ kikiendelea kusaka kocha wa kuinoa timu va taifa ya nchi hiyo “Black Stars’, idadi ya makocha wasiopungua 600 wanatajwa kutuma maombi ya kuhitaji kazi hiyo.

Nafasi kwa sasa hiyo ipo wazi baada kuamua kumtupia virago Chris Hughton kutokana na matokeo yasiyoridhisha ambayo timu hiyo iliyapata kwenye fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zinazoendelea Ivory Coast.

Ripoti zinafichua kuwa idadi kubwa ya makocha ambao wametuma wasifu wao GFA wanatoka Barani Ulaya, wengine Amerika Kusini na Kaskazini na wachache kutoka Asia na Afrika.

Miongoni mwa makocha ambao wanatajwa kuomba kazi hiyo ni Felix Magath aliyewahi kuinoa FC Bayern Munich ambaye muda mfupi baada ya Ghana kuweka hadharani mpango wa kusaka kocha mpya, meneja wake aliibuka hadharani na kusema kuwa kocha huyo anaitaka kazi ya kuinoa Ghana.

Jina lingine ambalo linapewa nafasi kubwa miongoni mwa hao waliotuma wasifu wao wa kuomba kazi Ghana ni Tom Saintfiet ambaye naye kwa sasa hana kazi baada ya kuachana na Gambia aliyoiongoza kufuzu fainali za ‘AFCON 2023’ mara mbili mfululizo ingawa mwaka huu aliishia hatua ya makundi.

Kocha wa timu ya taifa ya Mauritania, Amir Abdou naye ametuma maombi ya kuinoa Ghana huku akikiri kwamba ikiwa atapata fursa hiyo ni jambo kubwa na lenye thamani kwake.

“Nani ambaye hataki kuinoa Ghana? Fursa hiyo ikija niko tayari,” alinukuliwa Abdou ambaye ametoka kuiongoza Mauritania kufuzu hatua ya 16 bora kwenye ‘AFCON 2023’ kwa mara ya kwanza.

Kwa mujibu wa GFA, mchakato wa kumsaka kocha mpya wa Ghana hautochukua muda mrefu na vigezo vikuu wanavyoviangalia ni ufahamu wa kocha kwa soka la Ghana na rekodi ya mafanikio ya nyuma.

Enzo Fernandez kuikacha Chelsea
Makatibu Wakuu wakutana kujadili masuala ya Lishe