Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Deogratias Sangu amewataka Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata mkoani Kigoma kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo yao.
Sangu ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata mkoa wa Kigoma katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo amewataka watendaji hao kuimarisha usalama, amani na utulivu kwenye vijijini.
Amesema, “Viongozi na wataalam katika kutekeleza ufanisi na utekelezaji wa majukumu yenu na kupata matokeo tarajiwa nipende kusisitiza maneno yafuatayo: Kaimarisheni usalama, amani na utulivu, hakikisheni mnawashirikisha wananchi kikamilifu ili kusaidia kutoa taarifa kwenu na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye maeneo yenu” alisema Sangu.
Aidha, amewataka watendaji hao kuacha kuwa visababishi vya wananchi kukosa imani nao kwenye maeneo ya usalama kwa nafasi walizonazo badala yake wawashirikishe wananchi kwa kuwa nao karibu pia kwenda kutoa huduma kwa wananchi wao bila upendeleo, kushughulikia kero na malalamiko pamoja na kufuata kanuni za maadili na misingi ya haki katika utumishi wa Umma.
Akitoa maelezo ya awali kabla ya hotuba ya mgeni rasmi, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ibrahim Minja amesema watendaji hao wamepata mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kusimamia kwa weledi miradi ya maendeleo, kukusanya mapato na kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma katika utumishi wao.
Akitoa neno la shukrani, Afisa Tarafa Ilagala Wilaya ya Uvinza, Liwaza Thomas ameishukuru Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuwapatia mafunzo na kwamba watakwenda kuyafanyia kazi lakini pia watazingatia sheria na taratibu katika utendaji wao kwa kutoa haki kwa wananchi na pia Serikali itegemee matokeo makubwa kwao.
Mafunzo kwa Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata yalianza kutolewa mwaka 2023 na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo mpaka sasa mikoa 13 imefikiwa ambayo ni Songwe, Rukwa, Katavi, Njombe, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Kigoma.