Serikali Nchini, imesema tayari imeanza utekelezaji wa Mradi wa Maji Dambia – Haydom, unaolenga kunufaisha Vijiji 19 vilivyopo Mbulu Vijijini.
Waziri wa Maji, Juma Aweso ameyasema hayo hii leo Februari 9, 2024 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la mbunge wa Mbulu vijijini Flatei Massay aliyeuliza ni lini Mradi wa Maji wa Vijiji 19 maarufu kama (Dambia) utaisha.
Amesema Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa matenki 5 yenye jumla ya lita 2,675,000, ulazaji wa bomba kuu la kupeleka maji kwenye tenki umbali wa Kilometa 8.7, ulazaji wa mabomba ya usambazaji umbali wa Kilometa 357.5, ujenzi wa nyumba 1 ya mitambo (pump house) na ufungaji wa umeme, ujenzi wa ofisi ya chombo cha watumiaji maji (CBWSO), ujenzi wa vituo 192 vya kutolea huduma ya maji vyenye mfumo wa malipo ya kabla (prepaid water meters).
“Ujenzi wa Mbauti 4 (Cattle troughs) za kunyweshea mifugo pamoja na ufungaji wa pampu 4 za kusukuma maji unaendelea,” amesema Aweso
Amesema Mradi huo upo kwenye hatua za awali za utekelezaji ambapo unatarajiwa kukamilika Mwezi Oktoba, 2025 na kunufaisha wananchi wapatao 133,737.