Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) imemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuweka mikakati wa kurejesha fedha zilizokopwa kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kimkakati wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha. (KKK).
Maelekezo hayo yametolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Justin Nyamoga (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida. na kusema Kamati haijarishishwa na utekelezaji wa mradi huo mara baada ya kusomewa utekelezaji wake na namna ya urejeshaji wa fedha kwa waliopimiwa mashamba.
Kutokana na hali hiyo, Nyamoga alishauri na kumuelekeza Makurugenzi wa Halmshauri ya Manyoni kukaa na wataalamu wake kuweka mikakati ya urejeshaji wa mikopo ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha mashamba.
Amesema, “Fedha zilizotolewa na Serikali kwa Halmashauri hiyo kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha mashamba sio za msaada bali ni mkopo zinatakiwa zifanyekazi inayoonesha mafanikio, hivyo wekeni mikakati wa kurejesha na kumaliza deni ili Serikali itumie fedha hizo kukopesha Halmashauri nyingine.”
“Hakikisheni mnaweka utaratibu na mkakati mzuri ambao hautaharibu mipangilio mengine ya miradi inayotekelezwa Manyoni, ni vizuri kuangalia namna bora ya kuutekeleza huo mradi sababu mmebainisha kuwa mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha mashamba ni mzuri na ungekua na tija kwa sasa na hapo baadaye kwa Halmashauri na wananchi.”
Nyamoga ameongeza: “Kamati itaufuatilia huu mradi sio tu kwa kulipa deni mnalodaiwa bali itataka kujua una maendeleo gani kwa wananchi.”
Naye Mwenyekiti wa Wakulima wa Korosho, Bw. Rashid Madenge ambaye ni mnufaika wa mradi huo ameishukuru Serikali kwani kupitia mradi huo thamani yake ya ardhi imepanda.
Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ni moja ya halmashauri kadhaa zilizopewa mikopo wa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kimkakati wa kuongeza thamani ya ardhi kwa kupanga, kupima na kumilikisha.

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi: Majaji wapewa uhakika
Wananchi toeni maoni kwa ajili ya sera yenye tija - Waziri