Serikali Nchini, imewahakikishia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, kuwa inayachukulia kwa uzito mkubwa, maoni na mapendekezo yao kuhusu maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, wakati akifunga Kikao Kazi cha Mafunzo ya Uelimishaji kwa Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kusini na Watendaji wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) mjini Songea.

Amesema tayari inayafanyia kazi baadhi ya mapendekezo ya maboresho ya sheria yaliyotolewa na waheshimiwa Majaji kwenye kikao kazi kama hicho kilichofanyika mjini Bagamoyo mwezi Julai, 2023.

“Mapendekezo ya kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleshwa, tumeyafanyia kazi na tunataraji muswada wa marekebisho kuwasilishwa bungeni hivi karibuni,” alisema Ndalichako.

Awali akifungua mafunzo hayo mwishoni mwa juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani aliwahimiza waajiri nchini kujisajili WCF na kutoa taarifa za ajira za wafanyakazi wao ili kulinda haki za wafanyakazi hao pindi wanapopatwa na majanga wakiwa kazini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema Mahakama ya Tanzania ni wadau muhimu wa Mfuko huo katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa Mfuko unategemea maamuzi mbalimbali ya mahakama katika utekelezaji wake wa majukumu ikiwemo maamuzi ya kesi za mirathi.

MKUBA yawaneemesha Wavuvi, Wajasiriamali Tanga
Halmashauri yapewa ushauri mkakati urejeshaji mkopo wa Mradi