Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji iongeze kasi katika uwekezaji kwenye ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua pamoja na kujengeni mabwawa ya kukinga maji ili yatumike wakati wa kiangazi, kwenye ukame na kuzuia mafuriko.
Majaliwa amewaagiza viongozi wa Bodi za Maji wa Mabonde waongeze jitihada katika uhifadhi wa vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kutangaza maeneo hayo kwenye gazeti la Serikali kama maeneo tengefu ili kuyalinda kisheria.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo baada ya kufungua Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Taifa la Sekta Mtambuka kuhusu Usimamizi na Uendeshaji wa Rasilimali za Maji katika ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Amesema, “Bodi za Maji za Mabonde zitekeleze agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti Rafiki wa Maji katika Vyanzo vya Maji nchini iliyofanyika Tarehe 16 Novemba 2022 kwa kupanda angalau miti rafiki wa maji milioni 2.5 kwa mwaka.”
Majaliwa pia amezitaka Halmashauri zote nchini zijenge na kusafisha miundombinu ya kusafirisha ama kuondoa maji ya mvua katika maeneo yao ili kuzuia mafuriko. “Wizara ya Madini idhibiti uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji kuhimiza wachimbaji kuzingatia utunzaji wa mazingira.”
Kwa upande wa Wakala wa Misitu Tanzania, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wake wadhibiti upandaji wa miti mingi ya kibiashara katika vyanzo vya maji kwa kuwa miti ikikatwa eneo litabaki kuwa jangwa, piasuala hilo litekelezwe sambamba na kusitisha kutoa vibali vya kuvuna misitu kwenye vyanzo vya maji.