Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), imeipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuendeleza tafiti na bunifu zinazochagiza usanifu na utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA inayoleta tija kwa taifa.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya PAC, Japhet Hasunga, mara baada ya kamati hiyo kufanya ziara fupi ya kutembelea Kituo Cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGOVRIDC) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kilichopo jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Hasunga amesema kwamba, e-GA imewezesha serikali kuokoa fedha nyingi kwa kusanifu na kutengeza mifumo ya TEHAMA inayotumika katika taasisi mbalimbali za umma ambapo, hapo awali mifumo hiyo ilinunuliwa kutoka nje ya Tanzania kwa gharama kubwa.

“Moja ya jambo lililokuwa linatusumbua sana kamati hii ni taasisi nyingi kununua mifumo ya TEHAMA kutoka nje, lakini msimbo (source code) zinabaki kule kwa waliotengeneza mifumo na wakati mwingine mifumo hiyo baada ya muda haitumiki tena, na hivyo sisi tumekuwa tukisema hakuna thamani ya fedha katika ununuaji wa mifumo hiyo ambayo tumetumia gharama kubwa sana kuinunua,” amesema

Katika kuhakikisha mifumo ya TEHAMA Serikalini inawasiliana na kubadilishana taarifa, Hasunga ameitaka e-GA kuhakikisha kwamba taasisi nyingi zaidi zinaunganishwa katika Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini (GovESB), ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali mtandao kwa wananchi.

Naye mjumbe wa kamati hiyo, Mh.Ester Matiko, ameipongeza e-GA na kushauri Serikali kuwekeza zaidi kwa vijana ili kuwezesha nchi kuingia katika teknolojia za kisasa ikiwemo ‘blockchain’ na akilii bandia.

“Uwepo wangu hapa nimepata vitu vingi vya ziada ambavyo nilikuwa sivijui, hivyo niiombe Serikali na taasisi zake wawaangalie vijana hawa na wengine ambao wapo huko nje kuhakikisha tunawasaidia na wanatumika ipasavyo katika ujenzi wa Serikali Mtandao,” amesema Matiko.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ameiomba kamati hiyo kuwa mabalozi wa kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), katika kuhakikisha inakuza jitahada za Serikali Mtandao nchini.

Ameieleza kamati hiyo kwamba kituo hicho cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao kina eneo finyu hivyo, e-GA inahitaji kutengewa bajeti ili kujenga miundombinu (majengo) yake katika eneo la Kikombo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA, Mhandisi Benedict Ndomba, ameishukuru kamati hiyo kutembelea kituo hicho na kuahidi kutekeleza maelekezo, maoni na ushauri uliotolewa na wajumbe wa kamati hiyo ili kuimarisha bunifu na tafiti za Serikali Mtandao.

Mbowe akumbuka ushupavu wa Lowassa mpenda mabadiliko
Rais Samia kuongoza mazishi ya Lowassa