Kwa niaba ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA na Watanzania wenzangu, napenda kutoa salamu zangu za dhati, za Pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wapenda demokrasia wote kwa kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, kilichotokea leo tarehe 10 Februari 2024.
Lowassa alikuwa kiongozi shupavu, mwanasiasa mahiri, mwanaharakati hodari na alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini mwetu. Alikuwa rafiki yangu na mshirika katika safari ya kuleta demokrasia ya kweli Tanzania. Alikuwa mtu mwenye hekima, busara, ujasiri, uzalendo, mtu mwenye huruma, upendo na msamaha kwa wote.
Alikuwa mtu mwenye maono, mipango na mtekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi. Nimepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo chake. Nimepoteza rafiki, ndugu na mshauri mzuri. Tanzania na Dunia imepoteza kiongozi shujaa, mwenye mchango mkubwa katika kujenga amani, ushirikiano na ustawi wa jamii.
Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, amsamehe makosa yake na amjaalie rehema zake. Mungu aipe faraja, nguvu na subira familia yake, chama chake, wafuasi wake na wote walioguswa na msiba huu.
Tutaendelea kuenzi kazi, mawazo na hekima alizotuachia Mheshimiwa Lowassa. Tutaendelea kumuombea na kumkumbuka kwa mema aliyotutendea.
Mungu ailaze roho ya Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa mahali pema peponi. Amina.
Freeman Aikaeli Mbowe
Mwenyekiti wa CHADEMA.

Kinachoendelea katika msiba wa Edward Lowassa
e-GA wapongezwa endelezaji tafiti mifumo ya TEHAMA