Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alitangaza siku tano za maombolezo ya kitaifa na bendera kupeperushwa nusu mlingoti kuanzia Februari 10, 2024,  anatarajiwa kuongoza Mazishi ya Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Lowassa, yanayotarajiwa kufanyika Wilayani Monduli Mkoani Arusha Jumamosi Februari 17, 2024.
Waziri Mkuu ameyasema hayo hii leo Jumapilii, Februari 11, 2024 wakati akitoa taarifa ya ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay, Dar es Salaam.
Amesema, katika kipindi cha siku tano za maombolezo, Taifa litaendelea na shughuli za umma na kijamii sambamba na kushirikiana na wanafamilia katika ratiba ya msiba kama ilivyoandaliwa na kamati ya mazishi ya Kitaifa na wanafamilia.
Aidha Majaliwa ameongeza kuwa kabla ya mazishi hayo mwili wa Hayati Lowassa unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam na Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na kwamba Jumanne Februari 13, 2024 mwili wa Hayati Lowasa unatarajiwa kuangwa na viongozi na wananchi katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Jumatano Februari 14 mwili wa Hayari Lowasa utapelekwa katika Kanisa la KKKT Azania Front kwa ajili ya ibada takatifu na kuaga na Alhamisi Februari 15 mwili wa Hayati Lowassa utasafirishwa hadi jijini Arusha ambapo viongozi na wananchi watapa fursa ya kuaga katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.
Edward Lowassa alifariki jana (Jumamosi, Februari 10, 2024) wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam na tangazo la kifo chake lilitolewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.

e-GA wapongezwa endelezaji tafiti mifumo ya TEHAMA
MKUBA yawaneemesha Wavuvi, Wajasiriamali Tanga