Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, Dk Patrice Motsepe amesema kuwa karibu watu bilioni 2 duniani walikuwa wakiangalia fainali za 34 za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofikia tamati jana Jumapili (Februari 11) nchini Ivory Coast.
Fainali hizo zilifungwa rasmi kwa wenyeji Ivory Coast kutwaa Ubingwa wa Afrika kwa kuichapa Nigeria 2-1, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Alassarne Ouattara, Ebimpé unaochukua watazamaji 60,000 uliopo katika viunga vya Abidjan.
Motsepe amefichua hayo alipozungumza na waandishi wa habari, na kusema hayo ni mafarikio ambayo Waafrika wanatakiwa kujivunia.
“Wamekaribia watu bilioni mbili walioangalia AFCON 2023 duniani. Kwa kweli tunatakiwa kujivunia hilo kama Waafrika na mashindano yajayo huenda yakawa bora zaidi.
“Mafanikio ya Afrika yatategemea Afrika kuwa pamoja, kufanya biashara pamoja na katika soka, nchi kushindana na kucheza pamoja, ” amesema Motsepe.
Taarifa za vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti kuwa waandaaji wa mashindano hayo waliandaa viwanja sita vizuri kwenye miji mitano katika mashindano hayo ya bara.