Mshambuliaji mwenye asili ya Zanzibar, Amahl Pellegrino amekamilisha usajili kwa kujiunga na Klabu ya San Jose Earthquakes ya Marekani akitokea Bodo/Glimt ya Norway kwa uhamisho wa zaidi ya Sh.700 milioni akimfuata mwanasoka bora wa dunia, Lionel Messi.

Pellegrino ambaye ameondoka Ulaya akiwa miongoni mwa washambuliaji hatari, ameshindwa kuficha kwa kusema ubora wa Ligi ya Marekani kwa sasa ni miongoni mwa sababu ambayo imemsukuma kufanya maamuzi hayo.

“Nimecheza mpira Ulaya kwa miaka mingi, nadhani ni wakati sahihi wa kukabiliana na changamoto mpya sehemu nyingine. Ligi ya Marekani ni miongoni mwa ligi nzuri na zenye mvuto,” alisema.

Uhamisho wa Pellegrino kutoka BodoGie hadi San Jose Earthquakes umepokelewa vizuri na mashabiki pamoja na wachambuzi wa klabu hiyo.

Taarifa ya utambulisho wake ilieleza: “Akiwa na umri wa miaka 33, Pellegrino analeta uzoefu mkubwa na rekodi ya kuvutia ya kufunga mabao. Usajili wake unalenga kuimarisha safu yetu ya ushambuliaji, tunataka kushindana kwa kiwango cha juu ndani na kimataifa.”

San Jose Earthquakes ilionekana kuwa na pengo kwenye safu yake ya ushambuliaji baada ya kuondoka kwa Cade Cowell kwenda Chivas, hivyo kutua kwa Mzanzibar huyo kunatazamwa kama suluhu.

Wakati akicheza soka la kulipwa Norway, Pellegrino alishinda tuzo mbili za Kiatu cha Dhahabu na akatawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka mnamo 2023.

Dkt. Molle aionya jamii matumizi holela ya P2
Motsepe: Bilion mbili wameangalia AFCON 2023