Kabla ya kuwa mfalme alikuwa akifahamika kwa jina la Ras Tafari Makonnen, hapa namzungumzia Haile Selassie, ambaye kimaisha ya Dunia alizaliwa Julai 23, 1892 na kufariki Agosti 27, 1975. Katika uhai wake alipata kuwa Kaisari wa Ethiopia na jina lake hilo jipya alilopewa baada ya kuwa mfalme lilikuwa na maana ya Utukufu wa Utatu Mtakatifu.

Alifahamika pia kwa jina la Simba wa Yuda, Mfalme wa wafalme, Bwana wa Mabwana, Baba yake alikuwa akiitwa Ras Makonnen ambaye alikuwa ni Gavana wa Harar, mwenye familia ya watoto wapatao 11, Mkristo muumini wa dhehebu la Orthodoksi ya Ethiopia.

Mwaka 1907, Haille Sellasie akiwa bado kijana alipewa cheo cha Ugavana wa Jimbo la Sidamo na ilipofika mwaka 1911 akarithi nafasi ya gavana wa Harar.

Baada ya kifo cha Malkia Zauditu 1930, Ras huyu akapokea taji na cheo cha Negus Negeste chenye maana ya “mfalme wa wafalme” wa Ethiopia, kisha hapo ndipo alipoamua kujiita jina la Haile Selassie.

Hapo habari zake zikaenea kote duniani na kusababisha kuibuka kwa imani mpya ya Rastafari iliyopokea jina kutoka kwake, ingawa mwenyewe alibaki mwamini wa Kanisa la Orthodoksi, akiwa na daraja ya shemasi.

Hii ilipelekea Watu weusi wa Jamaika, ambao waliokuwa wajukuu wa watumwa wa asili ya Afrika kusikia kwa mara ya kwanza ya kwamba kuna Mwafrika anaheshimiwa na wafalme wa Ulaya, wakaona huyo atakuwa ni mwokozi aliyetumwa na Mungu kuja kuwakomboa watu weusi.

Sababu ya Jamii kirasta kutumia jina lake pamoja na mafundisho yake ni kutokana kuheshimiwa kwake pamoja na maono makubwa aliyokuwa nayo juu ya Bara la Afrika, ili kujikomboa katika utumwa wa kiakili kwa kujitambua vilivyo na ndio maana halisi ya mitazamo na imani za kirasta duniani kote.

Hata hivyo, Haile Selassie alifukuzwa nchini Ethiopia mwaka 1936 baada ya Italia kuvamia Ethiopia lakini wakashindwa, ndipo akarudi mwaka 1941 kwa msaada wa Uingereza iliyowaondoa Waiitalia nchini humo katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Hakika utawala wa Haile Selassie uliifanya Ethiopia kuwa kitovu cha Mataifa yote ya Afrika katika harakati ya kulikomboa bara zima kujipatia uhuru, hivyo kufanya umoja wa Mataifa huru ya Afrika kujengwa nchini humo katika jiji la Addis Ababa.

Lakini licha ya Haile Selassie kuheshimiwa Kimataifa bado ndani ya nchi yake maendeleo yalikwama hivyo kufanya raia wake kuchukizwa na utawala wake kutokana na shida mbalimbali zilizowakumba ikiwamo njaa.

Kati ya mwaka 1972 mpaka 1973 kulitokea njaa kubwa katika majimbo ya Wollo na Tigray ikafuatwa na mapinduzi ya kijeshi ya 1974 na kifo chake kikatangazwa Agosti 28, 1975 huku ikiwa haieleweki kama aliuawa au kama alikufa kutokana na ugonjwa.

Mabaki ya maiti yake yalipatikana mwaka 1992 chini ya sakafu ya choo cha jumba la kifalme alikokamatwa na jeshi la mapinduzi na badaye Novemba 5, 2000 mabaki hayo yalipewa mazishi ya kifalme katika kanisa kuu la Kiorthodoksi la Addis Ababa.

Serikali yakanusha Madiwani kukopwa Posho
Gamondi aihofia Simba SC Ligi Kuu