Klabu ya Manchester United imeorodhesha majina mawili ya mastaa wa Bayer Leverkusen, Jeremie Frimpong na Edmond Tapsoba wakihitaji saini zao kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini wanapata wasiwasi kutokana na Liverpool kumhitaji kocha Xabi Alonso, wanaweza kutibua mipango.
Licha ya kushindwa kufanya usajili wowote dirisha la Januari, Kocha Erik ten Hag anatarajia kupewa pesa za kutosha kwa ajili ya usajili kwenye dirisha lijalo, huku maboresha makubwa yakitarajia kufanyika kwenye safu ya mabeki ya miamba hiyo ya Old Trafford.
Maswali mengi yanaibuka kuhusu hatima ya mabeki Aaron Wan-Bissaka, Raphael Varane na Victor Lindelof wakati Jonny Evans akijiandaa kuondoka wakati mkataba wake utakapofika tamati, jambo hilo linaifanya Man United kuwafikiria mabeki Frimpong na Tapsoba kuja kuongeza nguvu msimu ujao.
Mabeki hao wamekuwa kwenye kiwango bora kabisa huko Leverkusen wakiisaidia timu hiyo kuongoza msimamo wa Bundesliga kwa tofauti ya Pointi tano dhidi ya FC Bayern Munich kwenye nafasi ya pili.
Frimpong alikuwa kwenye rada za kocha Ten Hag tangu kwenye dirisha la Januari, lakini sasa atafanya jitihada za kumsajili beki huyo wa kulia kwa ajili ya msimu wa 2024/25.
Jambo hilo litafanya mmoja kati ya mabeki Diogo Dalot na Wan-Bissaka auzwe dirisha lijalo.
Kwenye nafasi ya mabeki wa kati, Varane na Evans huenda wakafunguliwa mlango wa kutokea dirisha lijalo, hata Lindelof naye safari inaweza kumhusu, hivyo wanamtazama Tapsoba kama mbadala sahihi.
Lakini, kitendo cha Liverpool kumtaka Kocha Alonso akachukue mikoba ya Jurgen Klopp huko Anfiedl mwishoni mwa msimu, kunaweza kuwatibulia mipango Man United kwa sababu kocha huyo kutoka nchini Hispania anaweza kupendekeza kwenda na mabeki hao huko Merseyside.