Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania bara ‘Young Africans’, Miguel Gamondi, ameonekana kushtushwa na kasi ya Simba SC katika mechi za hivi karibuni, hivyo ameanza kufanyia kazi safu yake ya ulinzi ambayo imeruhusu nyavu zao kutikiswa katika mechi mbili zilizopita.
Katika mbio hizo za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huuu 2023/24, Gamondi amesema inabidi afanye kazi ya ziada katika safu yake ya ulinzi, kwa kuwa timu wanayokimbizana nayo (Simba SC), inaonekana kiwango chao kuwa juu baada ya mapumziko ya mwezi mmoja na usajili mpya uliofanywa na Wekundu wa Msimbazi.
Kikosi cha Young Africans kimerejea jijini Dar es salaam baada ya kumalizana na Tanzania Prisons kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, hiyo ikiwa ni mechi ya pili kuruhusu bao.
Young Africans waliruhusU bao katika mchezo dhidi ya Mashujaa FC kwa ushindi wa bao 2-1 wakiwa Uwanja wa nyumbani, Azam Complex na hivi karibuni na Tanzania Prisons kwa kuibuka ushindi kama huo.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Gamondi amesema licha ya kuvUna alama tatu katika michezo yao, lakini bado suala la kuruhusu bao katika michezo miwili anatakiwa kulifanyia kazi mapema kwenye safu yake ya ulinzi.
Amesema licha ya kupata ushindi, wamekuwa wakiruhusu nyavu zao kutikiswa jambo ambalo anaamini hapo baadae litakuja kuathiri, kwani wanaweza kupoteza au kupata sare kwenye moja ya mechi, ikawa ni hatari katika mbio zao za ubingwa kwa kuwa Simba SC inaonekana kuwa ya moto hivi sasa tofauti na ile aliyokuwa akiiona awali.
“Ligi imekuwa na ushindani mkubwa, timu zimefanya maboresho makubwa, tunatakiwa kujiandaa vizuri katika michezo yetu ijayo kuhakikisha tunafanikiwa kuvuna alama tatu, lakini tusiruhusu nyavu zetu kutikiswa.
“Inapotokea mpinzani anaanza kupata bao la mapema kabla yetu na wengi wao hupenda kupoteza muda, itakuwa ngumu, tunatakiwa kulifanyia kazi jambo hilo mapema kwa safu ya ulinzi kuongeza umakini,” amesema Gamondi.
Ameongeza kuwa anahitaji kufanya maboresho hayo mapema zaidi kwa kusahihisha kuanzia safu ya ulinzi akiamini nafasi ya ushambuliaji haina tatizo kubwa kwa sababu viungo na mawinga hufanya jukumu hilo la kufunga.
Gamondi amesema mechi ijayo wanarudiana na KMC FC mzunguko wa pili, ambapo katika mchezo wa raundi ya kwanza walishinda 5-0, lakini anaamini watabadilika na kuja kivingine hali ambayo analazimika kuandaa kikosi chake vizuri.
Young Africans itakuwa mgeni wa KMC FC Jumamosi (Februari 17) Ukiwa mchezo wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo utakaochezwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.