Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imetembelea Shule ya Sekondari Dodoma kujionea majaribio ya mfumo wa ufundishaji mubashara ‘Live Teaching’ ambao unawezesha wanafunzi wa shule nyingine nchini kuunganishwa na mwalimu anayefundisha katika Shule ya Sekondari Kibaha.
Akizungumza baada ya kujionea mfumo huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Denis Londo amesema wameridhishwa na mfumo huo huku akiipongeza Serikali kwa kuja na teknolojia hiyo ambayo inakwenda kukuza kiwango cha elimu nchini.
Amesema, “niipongeze Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, tumejionea shule nyingi zikijengwa, uwekezaji wa elimu bila malipo hadi kidato cha sita na sasa teknolojia hii ya wanafunzi wa shule nyingine kushiriki kipindi cha masomo na wenzao waliopo Kibaha Sekondari.”
Aidha, Londo aliongeza kuwa, “rai yetu kama Kamati ni kuitaka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuusimamia kikamilifu mfumo huu ili uweze kuleta tija kwa wanafunzi wetu nchini. Lakini niwatake wanafunzi hawa wanaonufaika na mfumo huu kuutumia kikamilifu ili waweze kufaidika nao kwenye masomo yao na kupata matokeo mazuri,”
Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde amesema wamepokea maelekezo ya Kamati hiyo na kwamba watahakikisha mfumo huo unatumika ipasavyo kama ilivyokusudiwa na kuwa wenye manufaa kwa wanafunzi nchini.