Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watumishi wa afya wazembe ambao hawatazingatia maadili, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na miiko ya kitaluma.
Dkt. Dugange ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa mwaka wa Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya Msingi ambao umelenga kujadili utekelezaji, mafanikio, changamoto na fursa katika utoaji wa huduma bora za afya, ustawi wa jamii na lishe kwa wananchi.
Amewakumbusha umuhimu wa kufanya kazi kulingana na maadili ya utumishi wa umma na taaluma zao na kuwambia kuwa, “tunaelewa kwamba kazi yenu inahusisha maisha ya watu na inaweka mzigo mkubwa wa dhamana kwenu. Ninatoa wito kwa kila mmoja wenu kujitahidi kuhakikisha kwamba anafuata sheria na miongozo iliyowekwa, kutenda haki na kuweka maslahi ya wateja mbele.”
Amesema, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watumishi wote wazembe ambao hawatazingatia maadili, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma na miiko ya kitaluma, huku akiwaelekeza wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba kila kituo kinafunga na kutumia mfumo wa kielektroniki ya kukusanya taarifa za afya, ustawi wa jamii na lishe ikiwamo wa GoTHOMIS ulioboreshwa.
Aidha, Dkt. Dugange amesema mpaka sasa vituo vya kutolea huduma za afya 1,564 kati ya 6,873 sawa na asilimia 22.8 vimefunga mfumo wa GoTHOMIS na kuwataka waganga wafawidhi kutatua changamoto za wananchi ipasavyo, kwa weledi na kwa wakati na wanafanyakazi kwa karibu na jamii kuhakikisha kuwa wanapata huduma stahiki.
Pia amewataka kuzingatiwa kwa utoaji wa huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo watu wenye ulemavu, wazee, na makundi mengine yenye mahitaji ya kipekee kwa kuwa na miundombinu rafiki na kutenga bajeti ya mahitaji maalumu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu kulingana na uhitaji, mafuta maalumu kwa watu wenye ualbino, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kuhusu kutunza na kutoa huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu.
Hata hivyo, Dkt. Dugange amewataka waganga wafawidhi kuhakikisha kuwa huduma za lishe zinatolewa kwa ufanisi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya jamii na kutenga bajeti za kuimarisha utoaji wa huduma za lishe ili kuendelea kupunguza matatizo mbalimbali ya lishe ikiwemo udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano.