Mshambuliaji kutoka nchini Uruguay Luis Suárez amesema Klabu ya Inter Miami ya nchini Marekani itakuwa ya mwisho kwake, kwani hatarajii kuendelea kucheza sola la ushindani baada ya kuondoka klabuni hapo.
Suárez mwenye umri wa miaka 37, alijiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Soka ya Marekani ‘MLS’, mwaka jana kwa msimu wa 2024 baada ya kuitumikia Gremio ya Brazil.
Aliungana na wachezaji wenzake wa zamani wa FC Barcelona, Lionel Messi, Sergio Busquets na Jordi Alba, ambaye alishinda nao mataji manne ya La Liga ndani ya miaka mitano nchini Hispania.
“Inter Miami itakuwa klabu yangu ya mwisho, familia yangu tayari inajua hilo. Sina tarehe bado, lakini ni hatua ya mwisho,” amesema Suárez katika mahojiano na kituo cha redio cha Uruguay Del Sol.
“Niko tayari kwa changamoto hii ya mwisho, lakini kuna uchovu usioepukika na mwishowe, nataka kuwa na maisha bora katika siku zijazo,” ameongeza.
Suárez, ambaye pia alizichezea Ajax Amsterdam, Liverpool na Atlético Madrid, amecheza mechi 138 akiwa na Uruguay tangu mwaka 2007.