Wakati Simba SC ikivuna Pointi 18 kati ya 21 kwenye michezo saba ya Ligi Kuu Bara ikiwa chini ya kocha Abdelhak Benchikha, kiungo fundi wa kikosi hicho, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ ameeleza kuwa bado wanaendelea kujifua ili kuwa bora zaidi.

Chama ambaye ameifanya Simba SC kuvuna Pointi nne kwenye michezo miwili kati ya mitatu iliyopita ya ligi kwa kufunga dhidi ya JKT Tanzania na Azam FC, amesema malengo kama timu ni kuchukua ubingwa, hivyo wataendelea kuweka mkazo kwenye kila mchezo na kufanyia kazi upungufu walionao ili kufanikisha hilo.

“Tangu tuanze tulikuwa na makosa madogo madogo lakini naona kama bado tunaendelea kujitafuta. Nafasi ya pili sio mbaya nahisi Young Africans wametupita Pointi nne. Kwa hiyo tutaendelea kupunguza utofauti huo kwa sababu malengo ubingwa wa ligi.” amesema mchezaji huyo.

“Mashabiki wa Simba SC wategemee mazuri kutoka kwenye timu, watuombee na kutusapoti na sisi tutaendelea kupambana kwa ajili yao. Tunaomba watupe sapoti,” ameongeza nyota huyo wa kimataifa wa Zambia.

Akizungumzia bao ambalo alifunga dhidi ya JKT Tanzania, Chama amesema anapokuwa uwanjani kwake kufunga sio kitu cha ajabu ambacho anakipa kipaumbele na wala huwa hajivunii, lakini jambo muhimu kwake ni kuona timu inapata matokeo mazuri kwenye kila mchezo maana unaweza kufunga halafu mkapoteza.

Kwa upande wake, Kocha Benchikha amesema anafurahi kuona fundi huyo amekuwa sehemu ya upatikanaji wa matokeo ambayo wameyapata kwenye michezo hiyo migumu ambayo ilifuata.

“Tumekuwa na ratiba ngumu lakini jambo muhimnu ni kwamba tumepata matokeo chanya, tunaendelea na safari, tunatakiwa kupiga hatua kama timu.”

Tangu Chama arejee kikosini akitokea kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ambazo zilifanyika nchini Ivory Coast akiwa na timu yake ya taifa la Zambia, ameinogesha Simba SC kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji.

Luis Suárez: Sitaendelea tena baada ya hapa
Makundi Ligi ya Mabingwa Mikoa hadharani