Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Batilda Buruani, ameonyeshwa kukerwa na tabia ya baadhi ya mashabiki wa soka mkoani humo kushangilia timu nyingine zinapokwenda kucheza kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi dhidi ya wenyeji, Tabora United.

Batilda amekiri kukasirishwa huko kufuatia mashabiki wengi kuonekana kuzishangilia timu za Simba SC na Namungo Fc zilipocheza mkoani humo hivi karibuni.

Kiongozi huyo amewataka mashabiki hao kujitathirni kama kweli wanahitaji kuendelea kushuhudia michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tunahitaji timu ya mkoa au tuendelee kuwa mashabiki wa klabu za Simba na Young?” alijohi kiongozi huyo wa mkoa.”

Amewakumbusha mashabiki wa soka wa Tabora hata kuziona klabu kubwa mkoani humo ni lazima kuhakikisha Tabora United inasalia kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Lakini ni lazima tujue ili Simba SC na Young Africans waje Tabora ni lazima kuwe na timu itakayowaleta wachezee kwenye Uwanja wa nyumbani, timu yetu ikicheza na kufunga bao mashabiki wanaoshangilia ni wachache, lakini kwenye hizi timu kubwa uwanja mzima unashangilia, sasa unajiuliza hii timu ya Tabora United inacheza Morogoro au Dar es salaam, ukweli ni aibu.

Yaani kweli tukubaliane kuwa Tabora ni ya Simba SC na Young Africans, tuendelee tu na ngoma zetu, kuhusu mpira tuendelee kushabikiwa timu kubwa tunazozijua?” amesema Batilda na kuwataka wabadilike.

Tabora United inatarajiwa kucheza dhidi ya Azam FC keshokutwa Jumatatu (Februari 19), hivyo mashabiki wametakiwa kuanza kuiunga mkono timu hiyo.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tabora United iko kwenye nafasi ya 14 ikiwa na pointi 17 kibindoni.

Juma lililopita, Tabora United ilikipiga dhidi ya Simba SC na kuchapwa mabao 4-0 kwenye uwanja huo, kabla ya kucheza dhidi ya Namungo FC na kuambulia sare ya bao 1-1.

Mbappe kusepa mwishoni mwa msimu
PSG yajiandaa kumtwaa Osimhen