Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe, ameiambia Paris St-Germain ana nia ya kuondoka katika klabu hiyo ifikapo mwishoni mwa msimu huu.
Mkataba wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 na mabingwa hao wa Ligue 1 unakaribia kumalizika na amekuwa akihusishwa kujiunga na Real Madrid.
Mustakabali wa Mbappe ulikumbwa na mzozo mkubwa na PSG msimu uliopita wa joto.
Wakati fulani, Mbappe alifukuzwa kwenye kikosi cha kwanza na kuachwa nje ya ziara ya klabu hiyo ilipokwenda kufanya maandalizi ya msimu mpya barani Asia.
Lakini makubaliano yalifikiwa ambayo yalihakikisha PSG haitapoteza wakati, Mbappe atakapoondoka na masharti ya kuondoka kwake ambayo sasa inaonekana haiwezi kuepukika.
Mshambuliaji huyo ana kipengele cha kuongeza mwaka mmoja, hivyo inatarajiwa kuondoka kwake kutahusisha ama mauzo na ada ya uhamisho au fidia za kifedha kwa upande wa mchezaji.
Ingawa PSG wangetaka Mbappe abaki klabuni hapo, kuondoka kwake kunaonekana kuja huku wakilenga kujenga kikosi cha vijana.
Inakadiriwa Mbappe, ambaye alishinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018, anapokea takribani euro milioni 200 kwa mwaka.