Kiungo mkabaji wa Young Africans, Mudathir Yahya, amesema siri kubwa ya kufunga mabao msimu huu ni baada ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi, kumwongezea majukumu ndani ya uwanja.

Kwa mara nyingine tena, juzi Jumamosi (Februari 17) Mudathir alifunga mabao mawili dhidi ya KMC, Young Africans ikishinda 3-0, huo ukiwa ni mwendelezo wa kufunga mfululizo baada ya mechi zilizopita kuifungia Young Africans 1-0 dhidi ya Namungo, Young Africans 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC na wakati wakiichapa 2-1 dhidi Mashujaa FC.

Mudathir, amesema kulingana na majukumu hayo anaamini ataendelea kufunga sana kwa sababu anatakiwa kukaba, kuchezesha na kazi kubwa kuhakikisha ashambulia kwa kufika katika boksi la mpinzani.

Amesema mabao sita aliyofunga ni kwa aina moja, baada ya kufuata maelekezo aliyopewa na Gamondi, kumtaka uwanjani kufanya majukumu yake na zaidi kupanda kushambulia kwa kufika ndani ya 18 ya mpinzani wanapokuwa na mpira.

Amesema jukumu la kuzuia pale wapinzani wanapokuwa na mpira anatakiwa kuhakikisha hawafiki katika eneo lao na kusababisha madhara, jambo ambalo amekuwa analifanya sana msimu huu chini ya Gamondi.

“Tangu nimeanza soka mwaka 2013, msimu huu nafunga sana, hakuna siri yoyote zaidi kujitoa na kujituma na kufanyia kazi mipango ya kocha ambayo anataka nijiongeze kwenye boksi, na ninafanya hivyo na kufunga.

“Gamondi ananipa majukumu yote uwanjani, kukaba, kuchezesha na kushambulia kwa kufika ndani ya boksi, nitafunga sana, nimeambiwa nifanye yote kwa sababu ya uwezo wangu wa kucheza nafasi nyingi wanjani,” amesema Mudathir.

Ameongeza kuwa hataki kumuangusha kocha wake kwa sababu amemwamini na kumpa nafasi, hali ambayo inamfanya kujitoa na kupambana kuhakikisha anaisaidia timu yake kuvuna pointi tatu katika michezo ya hiyo ya ligi kuu, na wiki hii wakielekea mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mudathir amesema anatarajia kuendelea kufunga katika michezo ya ligi hiyo kuhakikisha wanatetea taji lao la ubingwa na michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, kwa kutafuta pointi tatu dhidi ya CR Belouizdad watakaocheza Jumamosi wiki hii, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na Machi Mosi, mwaka huu nchini Misri dhidi ya Al Ahly.

Kiungo huyo amefikisha mabao sita huku akijiweka rekodi ya kuwa mkali wa kutibua mipango na kusaidia timu yake kuvuna pointi katika michezo migumu na muhimu.

Ujumbe wa NDC watembelea Wizara Mambo ya nje
Mashabiki waaswa KWA MKAPA