Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amekutana na Ujumbe wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) jijini Dodoma, hii leo Februari 19, 2024.

Ujumbe huo, uliokuwa ukiongozwa na Mkuu wa chuo hicho, Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge, ulipofika Wizarani ulishiriki mjadala kuhusu umuhimu wa Kuimarisha usalama wa jamii zinazoishi mipakani kwa ajili ya usalama endelevu wa Taifa (Enhancing Border Community Security for Sustainable National Security).

Ujumbe huo ulipokea wasilisho kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambapo Balozi Dkt. Shelukindo alielezea majukumu ya Wizara hususan katika kuhamasisha usalama mipakani.

Majukumu hayo yanahusisha uratibu wa mikutano ya ujirani mwema na Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPCs), Vituo Vya Utoaji Huduma Kwa Pamoja Mipakani (OSBPs), na kuratibu itifaki za kikanda na kimataifa.

Ujumbe huo wliokuwa na jumla ya washiriki 88, ulihusisha Wakufunzi 33, na Wanachuo 55 kutoka Tanzania na mataifa ya Afrika yakiwemo Nigeria, Namibia, Misri, Zambia na Zimbabwe upo katika ziara za mafunzo katika taasisi mbalimbali kwa lengo la kujifunza mchango wa taasisi hizo katika maendeleo ya nchi hususan kwenye sekta ya ulinzi na usalama.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Februari 20, 2024
Mudathir Yahya: Nitafunga sana msimu huu