Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema Serikali inaiangalia sekta binafsi kwa mtazamo chanya wa kuwa mdau muhimu wa uchumi na maendeleo.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Mkutano mkuu wa 15 wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar hii leo Februari 19, 2024.
Amesema, tayari kazi ya kuandaa sheria inayohusisha maendeleo ya sekta binafsi inaendelea chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ikisimamiwa na Sekretarieti ya Baraza la Taifa la Biashara.
Rais Mwinyi pia amemtaka Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe.Omar Said Shaaban kusimamia kukamilika kwa sheria hiyo mwishoni mwaka huu.
Amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kuitangaza Zanzibar katika majukwaa mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa kuvutia wawekezaji wengi zaidi ili kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeanzisha mifumo mbalimbali ya kurahisisha mazingira bora ya kufanya biashara nchini katika kuendana sambamba na maendeleo ya dunia ya sayansi na teknolojia ili kurahisisha huduma za maisha ya wananchi.