Vyombo vya Habari, vimehimizwa kuripoti kwa kina mapungufu ya sheria za Habari za Zanzibar, ili zifanyiwe marekebisho na kutoa fursa kwa Wananchi kupata taarifa mbalimbali bila vikwazo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika kikao cha uzinduzi wa ripoti ya mapitio ya sheria za habari zenye vifungu vinavyokwaza uhuru wa habari Zanzibar.

Amesema, “Waandishi wa Habari tutumie nafasi kupaza sauti zetu juu ya mapungufu ya kisheria yaliyopo ili zifanyiwe marekebisho, hii itawapa watu furaha na kujisikia kuwa ni sehemu ya nchi kwa kutoa maoni yao bila hofu.”

Dkt.Mzuri ameongeza kuwa, Waandishi wa Habari wakiwa na uwezo wa kutoa maoni yao bila hofu itarahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza uwajibikaji katika nyanja mbalimbali.

“Kukiwa na uhuru wa habari itasaidia kupunguza madhaifu yaliyopo kwenye sekta ya habari kwa kudhibiti waandishi holela wanaotoa taarifa feki na kuifanya sekta ya habari kuwa imara na kutoa taarifa ambazo zinakidhi misingi ya uandishi,” alisema.

Awali, akiwasilisha ripoti hiyo, Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar, Said Suleiman alisema uchambuzi wa sheria hizo umebaini uwepo baadhi ya vifungu vinavyokwaza uhuru wa Habari.

Aidha, aliongeza kuwa ripoti hiyo imepitia jumla ya sheria nane (8) ambazo ni Sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa marekebisho na sheria no.8 ya 1997, Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 iliyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010.

Nyingine ni sheria ya adhabu ya mwaka 2004 (Sheria Na. 6) iliyorekebishwa mwaka 2018, Sheria ya kufuta Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya mwaka 1984 na kutungwa kwa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2017 na mambo mengine yanayohusiana na hayo pamoja na Sheria ya Baraza la Wawakilishi Na 4 ya mwaka 2007 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Said ameendelea kufafanua kiwa, Sheria ya Tume ya Utangazaji Na. 7 ya 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria Na. 1, 2010 inahitaji kufanyiwa marekebisho kifungu cha 27 (2) kutokana na kutoa mamlaka zaidi kwa viongozi.

“Sheria ya Tume ya Utangazaji No. 7 ya 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria No. 1, 2010 viongozi wamepewa mamlaka makubwa sana mfano kifungu cha 27 (2). Waziri amepewa mamlaka makubwa sana ya kuchukua maamuzi yoyote,” alisema.

Aidha, alipendekeza sheria na sera kuwekewa vifungu vinavyoweka mazingira ya usalama wa waandishi wa habari ili kuwalinda dhidi ya uvunjifu wa uhuru wa kujieleza.

Kqa upande wake Mdau wa Habari, Jabir Idrissa alisema uwepo wa sheria zinazokwaza uhuru wa habari imepelekea Zanzibar kukosekana kwa vyombo vya habari binafsi kwa upande wa magazeti kutokana na urasimu katika utekelezaji wa sheria hizo.

“Mpaka leo Zanzibar hakuna Gazeti binafsi, ambapo kabla ya Mapinduzi kulikuwa na magazeti mengi Zanzibar, historia ya uandishi wa habari Zanzibar ni ya muda mrefu lakini imekufa kutokana na uwepo wa sheria zisizo rafiki,” alibainisha Jabir.

TAMWA ZNZ, kwa kushirikiana na wadau na Waandishi wa Habari Zanzibar wanaendelea kufanya ushawishi na utetezi wa mabadiliko ya sheria zenye vifungu vinavyokwaza uhuru wa Habari, wakilenga kupata sheria huru na zinazoendana na wakati.

Mashabiki Wydad AC waipigia magoti Asec
Al Ahly yakwama Accra