Kiungo kutoka Tanzania Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ amejiunga na klabu ya Konkola Blades ya Ligi Kuu Zambia na kuwa mchezaji wa tatu kutoka nchini kutua kwenye ligi hiyo katika kipindi hiki, baada ya Moses Phiri aliyekuwa Simba SC kujiunga na Power Dynamos na Idriss Mbombo aliyekuwa Azam FC kutua Nkana Red Devils.

Phiri alitua Dynamos kwa mkopo akitokea Simba SC akiwa ametoka kufunga mabao matatu kwenye Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, huku Mbombo ameachana na Azam FC akitoka kuifungia mabao manane msimu uliopita baada ya kuanza msimu huu akiwa majeruhi na kukosa namba mbele ya nyota wapya waliosajili na kukimbilia Nkana.

Kwa upande wa Humud ameanza kazi kwenye timu yake hiyo inayoshika nafasi ya 11, kwenye ligi ya Zambia yenye jumla ya timu 18, ikiwa na alama 26 ilizovuna katika mechi 11 baada ya kushinda tano, sare 11 na kupoteza tano.

Homud amejiunga na timu hiyo kama mchezaji huru lakini kabla ya hapo aliwahi kuzichezea timu mbalimbali ikiwemo Simba SC, Azam, Ashanti United, Mtibwa Sugar, Sofapaka (Kenya), Coastal Union, Real Kings (Afrika Kusini), Majimaji FC, Namungo na Fountain Gate FC, sambamba na timu ya taifa, Taifa Stars’.

Humud huenda akaanza kuitumikia timu hiyo mpya kwenye mechi za mashindano katika mchezo wa Ligi Kuu ya Zambia, keshokutwa Jumamosi (Februari 24) na chama lake litakuwa ugenini kuvaana dhidi ya Green Buffaloes.

Mastaa Barcelona kupigwa bei
Mbappe kuvuruga mfumo Real Madrid