Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mgulu wa Ndege iliyopo katika kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro, wapo kwenye hatari ya kukubwa na magonjwa ya milipuko kutokana na shule hiyo kukosa vyoo.
Wakiwasilisha kero hiyo kwa Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz Abood aliyefika shuleni hapo, Wanafunzi wa shule hiyo wamesema tangu shule hiyo ianzishwe haijawahi kuwa na vyoo vya Walimu na Wanafunzi jambo linalowalazim kutumia vyoo vya shule jirani.
Baadhi ya wanafunzi hao walilazimika kutumia mabango kufikisha ujumbe huo pamoja na changamoto nyingine kwa Mbunge Abood, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa Maji shuleni, uhaba wa Madarasa, umeme na Madawati.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Maria Mbuya amesema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo imepita miaka miwili na miezi nane ambapo hadi sasa inajumla ya Wanafunzi wapatao 1,127 na majengo ya madarasa manne huku ikiwa na darasa la kwanza hadi la saba waliohamishiwa kutoka shule jirani.
Kufuatia changamoto hizo Mbunge wa Morogoro mjini Abdulaziz Abood amejitolea kujenga vyoo vya walimu huku Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akitoa ahadi ya kujenga vyoo vya wanafunzi.