Boniface Gideon – Tanga.
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana – CMSA, imesema mwamko wa Watanzania kujiunga na Masoko ya hisa imeongezeka kwa kiwango kikubwa, hali iliyosaidia kupanda kwa thamani ya uwekezaji wa Masoko ya hisa na hatifungani na katika Sekta nzima ya Fedha nchini.
Afisa Mtendaji wa CMSA, Nicodemus Mkama aliwaambia hayo Wadau wa Maendeleo Mkoa wa Tanga, wakati wa uzinduzi wa Hatifungani ya Mamlaka ya Maji (Tanga UWASA).
Amesema, mfumo wa Hatifungani ni sehemu ya Masoko ya mitaji katika Sekta ya fedha inayowezesha upatikanaji wa fedha kwa muda mrefu ,na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wakati na kuwezesha makundi mbalimbali kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Fedha za kugharamia shughuli za maendeleo huweza kupatikana kwa kuuza hisa za kampuni (Shares),hatifungani za kampuni (corporate Bond),hati fungani za Serikali ( Government Bond)na vipande katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja (collective investment scheme) “alisema Mkama
Aidha, aliongeza kuwa Taasisi hiyo imepata mafanikio zaidi kwa kipindi cha miaka minne iliyopita ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko na mitaji imeongezeka kwa asilimia 31.2 na kufukia shilingi Tirioni 37 .3 katika kipindi kilichoishia January 2024 ikilinganishw na Tirioni 28.4 ya kipindi kilichoishia January 2021,
“Jumla ya mauzo ya hisa na hati fungani katika soko la hisa yameongezeka kwa asilimia 61 .6 na kufikia shilingi tirioni 9.3 kutoka trioni 5.8,vilevile thamani ya mfuko ya uwekezaji wa pamoja imeongezeka kwa asilimia 291.6 na kufikia tirioni 1.9,” alisisitiza Mkama.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliwashukuru Wadau wakiwemo CMSA kwakufanikisha kupata mradi huo wa hati fungani hiyo, ambayo itasaidia kuongeza ufanisi na upatikanaji wa maji katika jiji la Tanga pamoja na wilaya za Muheza, Pangani na Mkinga,
Amesema, “hatifungani itasaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Wilaya za Tanga jiji,Muheza ,Pangani na mkinga ambapo ,hali ya upatikanaji wa huduma ya maji itapanda ifikapo 2025 hadi asilimia 100 kutoka asilimia 96.”
Alisema wamepata uzoefu wakusimamia miradi mingi ya maji hivyo wanaamini mradi huo wa Hatifungani utatekerezwa na wananchi watapata fursa yakushiriki kwa kiwango kikubwa.
“Tunauzoefu wakusimamia miradi mikubwa ya Maji ,na sisi Wizara hatutokuwa kikwazo kwa Watanzania kupata Maji Safi na salama,tunatarajia kutekereza miradi mingi ya Maji na ifikapo 2025 changamoto ya Maji Mijini na Vijijini itakuwa imekwisha,tunataka tutimize lengo la Rais kwavitendo,” alisema Aweso.