Timu ya soka ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’, itashuka dimbari leo Ijumaa (Februari 23) kuikabili Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ katika mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Olimpiki, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Mchezo huo ni muhimu kwa Twiga kushinda nyumbani kujiweka kwenye mazingira mazuri pindi timu hizo zitakaporudiana Februari 27, nchini Afrika Kusini.

Twiga imefuzu kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake ‘WAFCON 2024’ zitakazofanyika nchini Morocco baada ya kushinda kwa zaidi ya miaka 10.

Kufuzu Fainali hizo kunaleta matumaini kuwa wataendeleza walipoishia kwa kufanya vizuri zaidi kwenye mchezo dhidi ya Banyana Banyana.

Aidha, Banyana Banyana ambao ni mabingwa wa WAFCON 2022 pia ni miongoni mwa nchi zilizofuzu kushiriki Fainali zitakazofanyika Morocco sambamba na Twiga Stars.

Wachezaji wa Twiga Stars; Fatma Issa na Stumai Abdllah wakiuzungumzia mchezo huo wamesema wamejiandaa vizuri na wako tayari kupambana kumaliza mechi nyumbani.

“Kitu ambacho tulikuwa tukizungumza na wenzangu ni kupambana kwa sababu tunajua ni mchezo mgumu sana na kila mchezaii ana morali ya kutosha, wajitokeze kwa wingi na sisi tutawafurahisha,” amesema Fatma.

“Nina imani kocha wetu anajua cha kufanya, tukimaliza mechi nyumbari ugenini hatutapata shida, Mungu atatusaidia na kwa juhudi zetu wenyewe tutashinda,” amesema Stumai.

Taarifa ya TANESCO yakataliwa Chalinze
Thamani ya hisa, hatifungani yapanda - CMSA