Scolastica Msewa, Chalinze – Pwani.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Chalinze, limekataa kupitisha taarifa za utekelzaji wa mradi ya ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Bagamoyo pamoja na ile ya Shirika la umeme Nchini – TANESCO,  baada ya kutoridhishwa taarifa zilizowasilishwa na taasisi hizo.

Akizungumza katika kikao cha robo ya pili ya mwaka wa fedha mjini Chalinze, Mwenyekiti wa Halmashauri, Hassan Mwinyikondo amesema kutokana na umuhimu wa miradi hiyo kwa Wananchi wa Chalinze na Wilaya nzima ya Bagamoyo taarifa zilizoandaliwa zilikuwa zikitia shaka.

Alisema, kuhusu ujenzi wa Chuo cha Veta Wilayani humo Baraza limepata shaka juu taarifa zisizojitosheleza zilizotolewa na Mkuu wa idara hiyo, Davis Moje na haiendani na fedha zilizoletwa na Serikali kuu kutokana na  hatua za ujenzi zilipofikiwa.

Kwa upande wa TANESCO, Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Chalinze alisema Wananchi wamekuwa na maswali mengi kutokana na kukatika katika kwa umeme mara kwa mara na wao Madiwani hawana maelezo sahihi ya kuwajibu.

Aidha, baraza hilo pia limemtaka wakala wa usimamimizi wa Misitu TFS, Halmashauri ya Chalinze kutoa majibu ya kero mbalimbali zinazolalamikiwa na Wananchi dhidi yao katika Baraza hilo, watakalo andaa kwakuwa Meneja wake hakuhudhuria bila taarifa.

Amesisitiza kuwa, Madiwani ndio wawakilishi wa Wananchi katika Halmashauri hiyo hivyo wanatakiwa kuwa na taarifa sahihi na zakutosha, ili waweze kuwafafamulia katika Kata zao kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo muhimu kwa Wananchi wa Chalinze.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash aliungana na Baraza hilo na kutoa maagizo juu ya maamuzi yaliyofikiwa na kwamba vyombo vya usalama vifuatilie miradi hiyo na kama kutabainika ubadhirifu wowote hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.

 

Gamondi afichua siri Young Africans
Twiga Stars kuivaa Banyana Banyana