Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema anajiona mwenye bahati kuifundisha timu inayoundwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa kama hiyo.

Gamondi amesema ingawa huu ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na miamba hiyo ya Tanzania Bara, lakini mpaka sasa anafurahishwa na mwenendo wao katika mashindano yote wanayoshiriki.

“Kuna vitu vingi vinanifanya nijivunie kuwa kocha wa Young Africans, kwanza ni mwenendo mzuri tuliokuwa nao kwenye mashindano yote, lakini kitu kingine cha muhimu sana, ni namna mashabiki wanavyoipenda na kuisapoti timu yao kokote inapokwenda nao wapo, ukweli hiyo inanipa nguvu ya kupambana na kuwapa furaha,” amesema Gamondi.

Kocha huyo ameeleza kuwa kitu kingine kinachomfanya ajione mwenye bahati ya kuifundisha timu hiyo ni ubora na ukarimu waliokuwa nao wachezaji wake.

Amesema kufanya kazi na watu wa namna hiyo inamrahisishia yeye kutimiza kazi yake kwa wepesi na kutimiza malengo ambayo wamekusudia kuyafikia mwishoni mwa msimu huu.

“Ukweli najivunia kufanya kazi na wachezaji wangu, wana ukarimu wa hali ya juu kitu ambacho kinafanya nitimize majukumu yangu kwa urahisi zaidi unapofanya kazi na wachezaji wa namna hii ni rahisi kushika kile ninachowafundisha na kufuata kwa urahisi falsafa zangu na ndio kinachofanyika hivi sasa,” amesema.

Kocha huyo raia wa Argentina amesema kwa mwenendo waliokuwa nao, anaamini watakuwa na msimu mzuri na ataendeleza kile kizuri kilichofanywa msimu uliopita na mtangulizi wake, Nasreddine Nabi.

Elimu ya manunuzi asilimia 30 yatolewa Bukoba
Taarifa ya TANESCO yakataliwa Chalinze