Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Angel Gamondi amekiri ana kibarua cha kuimarisha kikosi chake kutokana na ugumu wa mechi yao ya Mzunguuko watano wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya CR Belouizdad kutoka Algeria utakaochezwa kesho Jumamosi (Februari 24) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Gamondi amesema anafahamu vyema mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na kundi lao lilivyo na watashuka uwanjani huku kila timu ikihitaji pointi zitakazowaimarisha katika msimamo.

Gamondi amesema amewaandaa wachezaji wake kusaka ushindi na kuhakikisha CR Belouizdad hawafanyi mashambulizi ambayo yanaweza kuwapatia ushindi.

Kocha huyo amesema wachezaji wake wanatakiwa kupambana kuhakikisha wanafanikiwa kupata ushindi katika mchezo huo kwa sababu ameshapata mwelekeo mzuri katika mifumo yake ikiwemo kuanzisha mashambulizi kwa kutumia mawinga pamoja na viungo.

“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri, tumefanikiwa kusahihisha makosa yetu na tunatambua utakuwa mchezo mgumu ukizingatia tunahitaji ushindi, tunachokitafuta kwa sasa ni pointi tatu, baadae ndio tuanze kufikiria idadi ya mabao mengi,” amesema Gamondi.

Ameongeza wanawafahamu wapinzani wao pia wamekuja kwa ajili ya kusaka ushindi wa Ugenini, wanafahamu ubora wa safu ya ulinzi na ushambuliaji ya CR Belouizdad, hivyo wamejipanga kuwamaliza hapa nyumbani.

Kamwe amesema wanaendelea na hamasa kwa ajili ya kuhakikisha Mashabiki wanajitokeza kwa wingi Uwanjani ili kushuhudia timu yao inavyopambana kusaka ushindi na kuifanya safari ya kutafuta tiketi ya Robo Fainali ikamilike.

Naye Kocha Mkuu wa CR Belouizdad, Marcos Paquette, amesema wamejiandaa vizuri na wamekuja kutafuta matokeo chanya na ameweka wazi kundi lao halina ugumu kwa sababu kila timu inapambana kutafuta pointi tatu.

“Tumekuja kutafuta ushindi, tunatambua Ugumu wa mchezo huu, tumetoka kucheza mechi hivi karibuni na sasa tupo tayari kuvaana na Young Africans.” amesema Marcos.

Azam FC yawekewa mtego Mbeya
Zanzibar mwenyeji CECAFA Senior Challenge