Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko Februari 25, 2024 ameshuhudia kuwashwa kwa mtambo wa kwanza katika Mradi wa Julius Nyerere na kungiza megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Biteko amesema kuingia kwa megawati 235 kunafanya mgao wa umeme kupungua kwa asilimia 85 nchini.
Amesema, “Ninafurahi kusema kile ambacho tuliahidi kufikia tarehe 25 Februari tutakuwa tumeingiza umeme wa mtambo namba 9 kimekamilika.”
Aidha, ameongeza kuwa mtambo namba 8 unatarajiwa kukamilika mwezi Machi na kufanya jumla Megawati 470 kuingia kwenye Gridi ya Taifa.
“Kazi ilipaswa kukamilika mwezi wa sita lakini kutokana na msukumo uliowekwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umefanya kazi kukamilika kabla ya wakati,” alibainisha Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema pamoja na uwepo wa changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi Serkali itaendeea na jitihada za utunzaji vyanzo vya maji ili kuhakikisha maji kwa ajili ya uzalishaji umeme yanapatikana.