Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amewaagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba kuchukua maoni ya Wafanyabiashara na wawekezaji, ili kuboresha sera na sheria za kodi.

Makamu wa Rais, ametoa agizo hilo wakati akizindua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji jijini Dar es Salaam na kusema hatua hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Amesema, “kusanyeni na mtumie maoni ya wadau ili kuathiri upya mifumo ya kodi iendane na mabadiliko makubwa ya uchumi wa nchi.”

Kabla ya kufungua Kongamano hilo, Dkt. Mpango alitembelea mabanda ya washiriki wa mkutano huo akafurahishwa na utekelezaji wa maboresho ya mazingira ya uwekezaji na biashara nchini na hivyo kuipongeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji inayoratibu na kuhamasisha uwekezaji nchini.

Katika salamu zake kwa washiriki wa Kongamano hilo, Prof. Kitila Mkumbo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, alisema Tanzania imekidhi vigezo vyote vya nchi inayovutia wawekezaji.

“Uzoefu wa miaka 27 ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), unaonesha nchi inayovutia uwekezaji lazima ikidhi vigezo kumi, ambavyo ni amani na utulivu, mazingira ya kisera,” amesema Prof. Mkumbo.

Vigezo vingine alivyovianisha ni; Uwepo wa soko kwa bidhaa watakazozalisha wawekezaji, utulivu wa kiuchumi na utulivu wa fedha kwa ujumla, uwepo wa vipaji na nguvu kazi, ubora wa miundombinu, viwango vya chini vya kodi, gharama ndogo za kuajiri wafanyakazi, Uwepo wa ardhi, na uwepo wa fedha za kugharamia miradi ya uwekezaji wa ndani.

Jukwaa la Kodi na Uwekezaji ni fursa ya wafanyabiarasha na wawekezaji kutoa maoni na kushiriki mjadala unaolenga kuibua changamoto mbalimbali za kisera, kisheria ili kusaidia maboresho ya uwekezaji na biashara nchini.

Waliogomea chanjo ya Surua waishia Gerezani
Aliyejeruhiwa kwa risasi asimulia tukio, Polisi yatoa ufafanuzi