Wakati Simba SC ikitarajiwa kushuka dimbani Jumamosi (Machi 02), wachezaji wameahidi kucheza kufa aủ kupona kupata ushindi dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Simba SC itaikaribisha Jwaneng Galaxy katika mchezo wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Timu hiyo itaikabili Jwaneng Galaxy ikiwa na rekodi ya kulazimisha sare, katika mchezo wa raundi ya kwanza uliochezwa ugenini nchini Botswana.

Katika mchezo wa Jumamosi (Machi 02) Simba SC inahitaji alama tatu kufuzu Robo Fainali ya mashindano hayo, baada ya kutoka suluhu na Asec Memosas ya lvory Coast, mechi iliyochezwa ugenini mwishoni mwa juma lililopita.

Simba SC ipo nafasi ya pili ikiwa na alama sita sawa na Wydad Casablanca iliyopo nafasi ya tatu, Asec Memosas ikiwa imeshafuzu Robo Fainali kwa alama 11, wakati Galaxy inashika mkia baada ya kuweka kibindoni alama nne.

Wakizungumza kuhusu mchezo huo, nahodha msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema, wachezaji walifanya kikao na Benchi la Ufundi ambapo waliahidi kupambana kupata ushindi.

Amesema wanaendelea kufanya mazoezi na kufuata maelekezo ya Benchi la Ufundi kujiandaa kwa mchezo huo ambao Simba SC inatakiwa kushinda ili kufuzu Robo Fainali.

“Hatutaki kurudia makosa, tumejipanga kwa jasho na damu kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo na kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.” amesema Tshabalala.

Mlinda Lango Aishi Manula amesema wanajua Mashabiki na Wapenzi wa klabu hiyo wana matumaini na kikosi hicho, hivyo malengo ni kuwapa furaha.

Mchezaji huyo amesema mchezo utakuwa mgumu kwa timu zote mbili, lakini hawatakubali kufungwa wakiwa uwanja wa nyumbani.

“Wachezaji tunaendelea na maandalizi ya mchezo, tunahitaji kupata ushindi na kutinga robo fainali, hatutaruhusu kufungwa,” amesema Manula.

Naye Clatous Chama amesema walipata suluhu katika mchezo uliopita dhidi ya Asec, hivyo, mkakati ni kupata ushindi kwenye mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Jwaneng Galaxy.

“Tunawaahidi hatutakubali kupoteza mchezo, tutapambana kadiri tuwezavyo ili tupate ushindi na kutinga Robo Fainali,” amesema Chama.

Simba SC ilinza Kampeni ya Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/24, kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Asec Mimosas, ilitoka suluhu na Jwaneng Galaxy, ilifungwa bao 1-0 Wydad Casablanca, iliichapa mabao 2-0 Wydad Casablanca kabla ya mwishoni mwa juma lililopita kutoka suluhu na Asec Mimosas.

Simba SC, Young Africans wapewa waamuzi wa AFCON
Uvamizi wa shoroba chanzo Wanyamapori kusababisha maafa