Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo ameeleza kutoridhishwa na mwenendo wa kikosi chake katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2023/24.

Timu hiyo juzi Jumapili (Februari 25) ililazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons, matokeo ambayo yamefanya tofauti ya alama kati yao na vinara Young Africans kuwa sita na mchezo mmoja mkononi.

Kocha huyo kutoka nchini Senegal amesema pamoja na idadi kubwa ya mechi zilizobaki lakini si kitu rahişi kuiondoa Young Africans kileleni kutokana na ubora iliyokuwa nao hivi sasa.

“Inaumiza kuona unadondosha alama katika hatua muhimu kama hii, ingawa ndio mchezo wa mpira wa miguu ulivyo lakini sifurahishwi kabisa na hili. Kitu kikubwa tunatakiwa kuzidi kupambana ili kurekebisha makosa yetu na kuwaombea mabaya Young Africans” amesema Dabo.

Kocha huyo amesema yeye na wenzake wa Benchi la Ufundi wataendelea kupambana Uwanja wa mazoezi kurekebisha upungufu walionao kwenye mechi zilizopita ili kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi zijazo za ligi.

Amesema kitu kingine kinachowapa tabu ni namna ya kucheza mechi za mikoani ambazo wamekuwa wakikutana na upinzani mkali kiasi kwamba inawapa wakati mgumu kucheza kwenye ubora waliokuwa nao.

Mbali ya kuzidiwana Young Africans kwa alama na mchezo mmoja lakini timu hiyo ipo mbele kwa tofauti ya alama moja na michezo miwili dhidi ya Simba SC iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Februari 28, 2024
Deco: De Jong, Araujo hawauzwi