Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), ambayo ni mdau mashuhuri katika tasnia ya madini nchini Tanzania kwa zaidi ya miongo miwili, imekuwa mstari wa mbele kushughulikia uhaba wa ujuzi na ukuzaji vipaji ndani ya sekta hiyo.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, GGML inatajwa kuwa haijazingatia tu ubora wa utendaji kazi, bali pia kuwekeza katika nguvu kazi ya baadaye ya Tanzania.
Kwa kutambua umuhimu wa kuandaa wafanyakazi wa baadaye na kukuza vipaji, GGML, kwa kushirikiana na wadau wengine, ilitoa mchango mkubwa wa zaidi ya dola milioni mbili mwaka 2009 katika kuandaa mitaala kuandaa vijana wa Kitanzania kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Moshi.
Mpango huu umezaa matunda kwa miaka mingi, ambapo zaidi ya vijana 1,400 wamepata mafunzo ya uchimbaji wa kina kifupi juu ya ardhi, hivyo kusaidia kupunguza uhaba wa ujuzi katika sekta hiyo.
Hata hivyo, dhamira ya GGML katika kukuza vipaji inazidi mafunzo ya ufundi stadi. Mnamo 2009, kampuni ilizindua mpango wa kuajiri wahitimu ili kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo vikuu wasio na ajira, Programu ambayo ilikuwa na idadi ya wahitimu 12 kila mwaka hadi mwaka 2012.
Baada ya kusitishwa kwa miaka mitano, GGML ya 2017 ilirejesha programu ya mafunzo kwa vitendo, ikiwapa vijana wa Kitanzania uzoefu muhimu wa kufanya kazi ndani ya GGML kwa mwaka, huku ikiwaruhusu kubobea zaidi katika fani zao. Kati ya 2017 na 2023, GGML ilichukua wahitimu 194 kwenye programu yake ya mafunzo tarajali.
Katika kupanua mafunzo hayo, mwaka huu 2024, kampuni hiyo imekuja na programu iliyopewa jina la African Business Unit (ABU) ambayo ni zaidi ya program ya mafunzo Taraji ynayaotolewa kwa mwaka.
Katika progamu hiyo ya ABU, jumla ya wahitimu 10 wa mafunzo tarajali kwa mwaka jana wamechaguliwa kuendelea na program hiyo ambayo mbali na kupata mafunzo ya juu zaidi pia wamepata ajira za kudumu ndani ya GGML.
Menejea Mwandamizi wa masuala ya Rasilimali watu, Charles Masubi anasema dhumuni la kuwa na mafunzo hayo tarajali kwa wahitimu wa vyuo vikuu kwanza ni kushirikiana na serikali kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi stahiki.
“Lakini pili, kwetu sisi GGML ina maana kubwa zaidi ya hapo kwani tunaandaa wafanyakazi wetu wa baadae tunatengeneza vipaji ambavyo huwa tunavichukua baada ya kuvinoa kutoka kwa wahitimu na kuwaajiri.
“Mbali na kuwafundisha kwa mwaka mmoja, pia tunawapatia kila maarifa wanayohitaji kwenye eneo lao la utaalam kama ni mhandisi tunahakikisha tunamfundisha na kumpa maarifa yote kwa vitendo akisimamiwa na wahandisi wabobevu,” anasema.
Masubi anasema program hiyo ya ABU inawajumuisha wahitimu wa vyuo mbalimbali waliomaliza progamu ya mafunzo tarajali kwa mwaka mmoja ndani ya GGML.
Hii ina maana kuwa baada ya kumaliza mafunzo hayo tarajali wahitimu waliofanya vizuri wanaunganishwa na waliopo kwenye migodi mingine ya Afrika ambapo wanafanya program kama hiyo ya GGML.
“Kisha tunawapa mafunzo ya juu zaidi ya ujuzi au juu ya elimu yao ya darasani, kama ni mhandisi tutamfundisha kuweka vipaumbele, makubaliano, kuandaa bajeti kupata ujuzi wa namna ya kuwasiliana kwa usahihi na wenzake. Kwa sababu vyote hivyo ni muhimu katika kufanya kazi,” anasema Masubi.
Anasema waashiriki wa program hiyo ya ABU, watashirikiana na migodi ya Afrika iliyo chini ya kampuni mama ya AngloGold Ashanti kwenye nchi za Ghana, Guinea.
“Wote watakuwa kwenye program inayofanana na lakini bado wakiendelea kubobea zaidi kwenye fani zao na kufanya mzunguko wa kujifunza zaidi kwenye migodi mingine.
“Hawa watu hatuwaandai kuishia kuwa wafanyakazi wa ngazi za chini, wakati mwingine tunawaandalia fursa ya kupanda juu na kuwa viongozi wakubwa wa kampuni haopo baadae,’ anasema Masubi.
“Tunapokuwa na programu ya pamoja tunatengeneza kiongozi ambaye atafahamu mila na desturi zetu za kazi kama kampuni, utamaduni wetu wa kazi, miiko yetu kila kitu kuhusu kampuni kwa hiyo ikitokea kiongozi huyu amepata nafasi kufanya kazi Ghana atakuwa na ufahamu wa kutosha.
“Atakwenda akiwa ameiva kwenye nyanja zote tunazozingatia AngloGold Ashanti mfano masuala ya uhasibu, uhandisi, mawasiliano, lazima awe vizuri kwa hiyo anakuwa mtaalam ambaye anaweza kuwa kwenye idara yoyote na kufanya kazi vizuri na kukua. Hilo ndio lengo kubwa la kuanzishwa kwa ABU,’ ameongeza Masubi.
Mmoja wa wahitimu hao, Diana Laswai ambaye mbali na kuishukuru GGML pia waliishukuru Serikali kwa kuendelea kuhamasisha sekta binafsi kutoa mafunzo kazini kwa vitendo na alitoa wito kwa wanafunzi wapya wanaoanza mafunzo hayo mwaka huu kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia nidhamu na kuzingatia tunu za GGML ambavyo ni usalama.
Evelyne Julius ambaye ni Mhandisi wa masuala ya umeme naye anasema “nimejifunza vitu vingi. Uwepo wangu GGML ni fursa ya kipekee kwa sababu nitaweza kutekeleza miradi mbalimbali kwa ujasiri na ujuzi nilioupata,” alisema.
Mkunde Frank, ambaye ni mteknolojia wa masuala ya jiolojia, naye anasema nafasi aliyoipata ya kuendelea kufanya kazi ndani ya GGML kupitia progamu ya ABU, imeendelea kumjengea kujiamini na kunoa zaidi ujuzi wake.
“Mathalani kwenye kitengo cha geolojia tumepata fursa ya kipekee, kila mfanyakazi anapewa uthamani bila kujali mkubwa au mdogo. Lakini hata ukishuka kwenye machimbo chini ya ardhi kila mfanyakazi anazingatia mafunzo aliyopewa kwa vitendo hasa katika kutekeleza kipaumbele cha kwanza ambacho ni usalama,” anasema.
Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Ujuzi kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Albert Rukeisa anasema hitihada hizo za GGML kwa zaidi ya miaka 15 zimekuwa chachu kwa waajiri wengine kuendelea kutoa nafasi kwa vijana kujifunza na kuongeza wataalam wa madini katika sekta hiyo.